Maswali na Majibu KCSE Kiswahili
Ufahamu | Ufupisho | Isimu Jamii | Insha | Utumizi wa Lugha
1. UFAHAMU (Alama 15) Soma habari iliyopo, kisha jibu maswali yanayofuatia. Kigumba kwa Nguruwe. Kikamilifu methali hii ni: Kigumba kwa nguruwe kwa mwanadamu ki chungu. Kufahamu maana yake, ni lazima tuchunguze kijuujuu maana ya maneno yaliyotumiwa. Kigumba ni chembe cha mshale, mkuki au chusa kinachotumiwa kuchoma na kumjeruhi mnyama. Nguruwe ni mnyama anayesakwa na kufumwa na kufurahikiwa na wasasi anapopatwa. Uchungu ni maumivu yanayoletwa na kitendo hicho cha kufuma. Nguruwe hufisidi mimea ya wakulima. Hapo basi husakwa kwa mishale na mikuki na kuuawa. Watu hupata uhondo wa nyama. Wakati mwingine, katika zile hekaheka za kusaka, huenda mshale au mkuki ukamdunga mtu badala ya yule mnyama.Vivyo hivyo anapaswa afahamu kuwa uchungu anaousikia yeye ndio ule aliousikia nguruwe. Mzee Kisheta alikuwa mraibu wa bangi, na kwa sababu hiyo, hakuweza kumkimu yeyote; si mkewe, si watoto hata mwenyewe na aila yake yote. Kila hela aliyoipata, alilongeza katika vihindo vya wauzaji bangi. Mkewe, Kitete, alikuwa akienda kutafuta vibarua angalau awasitiri wanawe. Chochote kile alichopata, ilimbidi akifiche, kwani mumewe alivisaka vibetini, mitoni na matandikoni, chini ya mivungu ilimradi nyumba nzima aliichakura. Akikipata hukimbilia kwa wachuuzi wake. Asipokiona, humkabili mkewe kwa matusi na magumi. Mkewe, aliyechekelea sana kufufutwa, humtolea nusu ya pesa alizopata ili aipoze ghaidhi ya mumewe. Kisheta huchomoka huyoo! Hapo basi Kitete huepukana na kero. Siku moja, Kitete alirudi na shilanga lake begani huku akitabasamia mwanawe mdogo Kita, aliyeuona uso wa furaha wa mamaye uliobashiri mafanikio aliuliza, “Mama una furaha leo! Je, umetuletea nini?” Mamake alimjibu kuwa alikuwa na furaha sana siku ile kwa sababu bibi aliyemlimia ngwe siku hiyo alimpa bahashishi ya shilingi ishirini kwa kazi yake nzuri. Badala ya shilingi hamsini alipata shilingi sabini. Ilikuwa furaha iliyoje! Alipomaliza kumjibu mwanawe kwa furaha, aliliingiza jembe lake ndani na kutoka haraka haraka awahi kwenda madukani kabla ya Kisheta kufika pale na kumnyang`anya pesa zake alizozipata kwa jasho. Alipotoka nje ya nyumba tu, alikutana na mumewe aliyezuka ghafula, haijulikani kutoka wapi! Papo hapo alimtolea jicho mkewe mkono kaunyosha akitaka kupewa ujira wote alioupata siku hiyo.Mama Kita alikataa katakata akisema hakupata chochote siku ile. Kisheta alikuja juu, akamshika mkewe akitaka kumvunja kama ukuni mkavu. Mkewe alilia kwa uchungu akijaribu kujikwamua, lakini mikono yake Kisheta ilikuwa imemkaba kama koleo. Hakuweza kumtoka. Mwanawe, Kita, alipomwona mamaye alivyokuwa akiteseka alisema, “Mama, kwa nini ufe na pesa unazo? Si umpe baba hizo shilingi sabini ulizozifunga hapo katika pindo la leso?” Kusikia hivyo, Kisheta alimwachilia mkewe kwa kumkita chini na kumwamrisha ampe pesa zile. Bibi huyo hakuwa na la kufanya ila kuzitoa. Kisha akakaa chini na kujiinamia kwa huzuni. Mzee Kisheta alifurahi na kumnyanyua Kita juu na kusema. “Wewe u dume kweli! Unampenda baba yako. Kua mwanangu na uwe kama babako.” Mtoto huyo alisikiza maneno hayo, lakini hakuonekana kuelewa aliyoambiwa. Siku nyingi zilipita na maisha ya Kisheta yalizidi kuzorota. Jumapili moja baada ya kupotea kutwa nzima, asijulikane alikokuwa. Kisheta alirudi akiandamana na watu wawili hadi pale nyumbani kwake. Walipofika mkabala wa ukumbi, Kisheta alisikika akisema, “Mabwana, mimi asilani sivuti hata sigara, lakini ikiwa mwasisitiza kuwa mwataka kuingia ndani basi mwakaribishwa.” Kita aliposikia babake akisema hivyo, alidakia, “Wewe baba huvuta sigara. Hata jana ulinituma sigara sita kubwa dukani kwa Ali.” Kisheta alimrukia Kita akataka kumzaba makofi. Kumbe wale mabwana aliokuwa nao walikuwa askari kanzu. Walimzuia asimpige mtoto; walilisaka banda lake la nyumba na kuona vipande sita vya misokoto ya bangi chini ya sanduku la mbao lililokuwa na suruali moja iliyojaa viraka na fulana moja kuukuu. Kisheta alitiwa pingu na kupelekwa kwenye kituo cha polisi. Alipokuwa akitolewa mle nyumbani, aliropoka laana kwa mwanawe Kita. Mama Kita matumbo yalimsokota akamkabili mumewe na kumsuta. “Msalie Mtume? Usinilaanie mwanangu? Malipo ni hapa duniani. Jambazi we! Umepata stahili yako!” Maswali: 1. Toa fasili ya kigumba katika kisa hiki. (Alama 2) ………………………………………………………………………… 2. Eleza uhusiano kati ya Kisheta na mkewe katika hali yao ya maisha. (Alama 3) …………………………………………………………………… 3. Ni kitu gani kilichopandisha mori Kisheta hata akawa karibu kumwumiza mkewe? (Alama 1) ……………………………………………………… 4. Taja sababu zilizomfanya mtoto Kita kutoboa kuwa mamaye alikuwa na pesa na babaye alivuta sigara? (Alama 2) ………………………………………………… 5. Ni mafunzo gani tunayoyapata kutokana na kisa hiki? (Alama 3) ………………………………………………… 6. “Kutojua ni usiku wa giza.” Fafanua msemo huu ukilinganisha na makala uliyosoma. (Alama 2) …………………………………………………… 7. “Jambazi we! Umepata stahili yako!” Fafanua. (Alama 2) …………………………………………………… MWONGOZO WA KUSAHIHISHA 1. Ni jambo la kuudhi unalolitendea mtu huku ukidhani huwezi kutendewa (alama 2) 2. • Kisheta alikuwa mkali • Kisheta hakumwamini mkewe • Kisheta hakumsaidia mkewe kwa chochote • Mkewe alikuwa mnyenyekevu kwake. 3. Kukatazwa pesa au pato la siku hiyo. 4. • Mama kita alirudi akitabasamu mpaka huyu mtoto akajua kulikuwa na mafanikio fulani. • Kita alifichua kuwa babake alikuwa amemtuma sigara kubwa dukani kwa Ali. 5. Hakuna siri ya watu wawili. - Kuna hatima ya mateso. - Familia haiwezi kuendelea utengano ukiwepo. 6. Kisheta alimdunisha mwanamke kwa kila alichofanya akidhani hakujua. • Kisheta alimshangilia mwanawe bila kufahamu kuwa ndiye angemtia matatani. 7. Mkewe alifurahia kilichotokea hata kama hakikuwa bora kwa mumewe. - Mkewe Kisheta hakuwa na uwezo wa kumkabili mumewe lakini neema za Mungu zilimwokoa akalipishiwa kisasi. Tanbihi i) Pitia majibu huku ukidondoa makosa ya - Sarufi - hijai ii) Kila kosa la sarufi litokeapo mara ya kwanza liondolewe nusu alama mpaka upeo wa aina kumi na mbili ½ x 12 alama 6 iii) Kila kosa la hijai liondolewe nusu alama hadi upeo wa aina sita za makosa ½ x 6 alama 6 Mfano J = 10 S = 1 (makosa mawili tofauti) 9 H = 2 (makosa manne tofauti) 07
0 Comments
Leave a Reply. |
Categories
All
Archives
July 2024
|
We Would Love to Have You Visit Soon! |
Hours24 HR Service
|
Telephone0728 450425
|
|
8-4-4 materialsLevels
Subjects
|
cbc materialsE.C.D.E
Lower Primary
Upper Primary
Lower Secondary
Upper Secondary
|
teacher support
Other Blogs
|