Maswali na Majibu KCSE Kiswahili
Ufahamu | Ufupisho | Isimu Jamii | Insha | Utumizi wa Lugha
FASIHI SIMULIZI - Soma utungo huu na kujibu maswali yanayofuata MODEL14122022002
Zamani sana katika kijiji cha Tima paliondokea sonara mmoja. Sonara huyu alikuwa na mke mrembo ambaye alihusudiwa na walimwengu wote katika eneo hilo. Karibu na kibanda chao palikuwa na msitu ambao ulisetiri mazimwi ya kila aina. Kila jioni ungeyasikia mazimwi hayo yaking’ang’ania mawindo. Sonara na mkewe hawakwisha kushangaa jinsi viumbe hawa walivyokithiri kwa tamaa.
Siku moja sonara aliondoka kijijini kwenda mbali kwa shughuli za ufuaji. Alimwacha mkewe akiwa mjamzito. Mara tu baada ya kuondoka, uchungu wa uzazi ulibisha hodi. Mama mtu akawa taabani, asiwe na mwombezi. Katika hali hii ya hamaniko, mama mtu alishutukia kapata mkunga aliyeonekana mzuri na mpole ajabu. Mama akajawa na furaha tele. Bahati iliyoje!
Mkunga akaingia kazini. Baada ya dakika chache, malaika, kitoto kichanga kikahanikiza hewa ya asubuhi mbichi kwa kilio. Mama mtu alishukuru mkunga kwa usamaria wema. Laiti angalijua kuwa kajipagaza zigo lisilobebeka!
Mkunga huyu hakukawia. Akaingia ghalani akachukuwa mtama. Akasaga na kumpikia mwanagenzi fuka. Mzazi, hamu ya kula hajapata bado, mkunga akamkabidhi bakuli la uji. “Shika mke mzazi”, akasema. Hata kabla ya mama kutoa kauli, mkunga akabadilika ghafla. Ile sauti ya upole ikabadilika kuwa mngurumo wa kutisha: “UKIKATAA, MIMI NAENDA KUUNYWA!”. Kumbe yule mkunga alikuwa zimwi lililobugia uji pamoja na bakuli! Mama alipoona hayo, vimbimbi vikamsimama kwa woga.
Kufikia jioni, njaa ilikuwa imemuuma mama na mtoto si haba. Yule mkunga zimwi akajigeuza binadamu na kumchinja mbuzi ili ampikie mama mzazi. Baada ya supu kuiva zimwi likaibeba pamoja na minofu na kumpelekea mama mzazi. Lakini hata kabla ya kutua sufuria, lilikariri maneno yale yale: “UKIKATAA NAENDA KUNYWA”. Kwa kauli hiyo, likabugia nyama pamoja na sufuria. Mbuzi mzima akapata makao ndani ya tumbo la zimwi! Mama na mtoto wake wakalala mataya yakigongana. Siku tatu zilipita bila ya mama kupewa chakula chochote. Unyonge wa uzazi ukamvamia, kitoto nacho kikaendelea kudai haki.
Asubuhi moja Kasuku alipatia akitarajia kiamsha kinywa kama kawaida. Akampata mke wa sahibu yake taabani. Baada ya mazungumzo mafupi na mama mtu, waliafikiana kuwa ampelekee sonara ujumbe.
“Kasuku alienda akatua juu ya mti uliokuwa karibu na kiwanda cha sonara. Akaimba:
Ewe sonara unayefua Mke kajifungua Unyonge wa uzazi wamaliza Tumbo la uzazi latekenya Chango zamsokota Kisa na maana Chakula hapati Mpishi hupikia tumbole Zimwi huchumia chunguche Kikawia hasara takufikia Ya kinda na mamaye
Sonara alisikiliza wimbo huu kwa muda na ujumbe wake ukamgonga ndipo. Akajihami na kufunga safari kurejea nyumbani. Alipofika, alimpata mkewe taabani, mwili umenyong’onyea. Magala yote yalikuwa yamefagiwa na zimwi lililokuwa limejidai kuwa mfadhili na lililala nje ya ghala kwa mavuno ya shibe. Sonara alilidunga mkuki likafa papo hapo. Ingawa sonara alijuta kwa kutowazia hali ya mke wake tangu awali aliweza kuliangamiza zimwi. Hadithi yangu inaiishia hapo.
Maswali
(a) (i) Tambulisha aina ya utanzu huu. (alama 1)
Hadithi/masimulizi (1x1=1) (ii) Taja tanzu zingine zinazoingiliana katika kifungu ulichosoma huku ukitolea mifano. (alama 2) ● nyimbo ● semi ● mazungumzo (3x1=3)
(b) “Hadithi yangu inaishia hapo”
Eleza umuhimu wa kifungu hiki katika uwasilishaji wa utungo huu. (alama 4) Fomyula ya kufunga; i) Huashiria mwisho wa ngano ii) Hutangaza funzo kwa wasikilizaji iii) Kuwapa changamoto ya kuwa watambaji mashuhuri wa ngano. iv) Humpisha mtambaji anayefuata v) Kuitoa hadhira ulimwengu wa hadithi (Sanaa) na kuwarudisha katika ulimwengu halisi. vi) Hupisha shughuli inayofuata vii) Ni kitulizo kwa hadhira ambayo sasa huacha kuwa makini. (5 x 1) = 5
(c) Jadili mafunzo yanajitokeza katika usimulizi huu. (alama 2)
i) Tuwe na mipango madhubuti maishani / tuyape mambo muhimu nafasi ya kwanza. Sonara alimwacha mkewe akiwa karibu kujifungua. (Hakuwajibika). Anajipata akiteseka sonara akiwa mbali naye. ii) Tutende wema daima. Jitu linauliwa na Sonara kutokana na ukatili walo. (1 x 2 = 2)
(d) Eleza namna ambavyo hadhira inaweza kushirikisha katika usimulizi huu. (alama 4)
- Kuimba - Kupiga makofi - Kuuliza maswali - Kuigiza - Kuitikia na kuhimiza - Kutoa mifano - Hisia/ishara za usoni ili mwasilishaji abadilishe uwasilishaji - Kutoa majibu - Kutoa mifano ya baadhi ya wahusika katika jamii zao endapo wataulizwa. - Kuchukua nafasi na kuitamba upya hadithi. (4x1=4)
(e) Kwa kutolea mifano orodhesha tamathali za usemi zilizotumika. (alama 4)
● Takriri - Ukikataa mimi naenda kunywa ● Kupiga chuku/ongezea chumvi - mbuzi mzima akapata makao ndani ya tumbo la zimwi. ● Tashihisi - unyonge wa mzazi ukamvamia. ● Jazanda - kinda kwa maana ya mtoto. ● Semi - chango zamsokota ● Nahau - funga safari [Tathmini jibu la mwanafunzi 4x1=4]
(f) Jadili aina za taswira zilizotumika na mtunzi. (alama 3)
Taswira sikivu - ungeyasikia mazimwi hayo yaking’ang’ania chakula - sauti, “ukikataa mimi naenda kunywa” Taswira oni - alikuwa mke mrembo Taswira mwendo - akaingia ghalani - asonara ujumbe - akajihami na kufunga safari Taswira hisi - akapata makao ndani ya tumbo la zimwi - ujumbe ukamgonga ndipo - mama akajawa na furaha tele - hakwisha kushangaa - uchungu wa uzazi ulibisha hodi (3x1=3)
0 Comments
Leave a Reply. |
Categories
All
Archives
July 2024
|
We Would Love to Have You Visit Soon! |
Hours24 HR Service
|
Telephone0728 450425
|
|
8-4-4 materialsLevels
Subjects
|
cbc materialsE.C.D.E
Lower Primary
Upper Primary
Lower Secondary
Upper Secondary
|
teacher support
Other Blogs
|